Askari wa Uhuru - Sehemu ya 1
Askari wa Uhuru • Hassan Bakari
Asubuhi ile ya Jumamosi, jua lilikuwa bado halijachomoza vizuri pale Buza. Mama Rehema alikuwa ameshaamka mapema kama kawaida yake, akiandaa chai ya tangawizi kwa watoto wake watatu. Nyumba yao ndogo lakini safi ilikuwa imeezekwa kwa bati, na upepo wa asubuhi ulipita kwa upole kupitia madirisha yaliyokuwa wazi.
"Watoto! Amkeni! Chai iko tayari," sauti yake ilivuma kwa upole lakini kwa nguvu ya mama anayejua jinsi ya kuamsha watoto wake. Mwanae wa kwanza, Juma, alikuwa wa kwanza kutoka chumbani. Kijana wa miaka kumi na nane, mrefu kama baba yake marehemu.
"Mama, leo naenda sokoni mapema," Juma alisema akinywa chai yake haraka. "Bibi Tatu ameniahidi kazi ya kubeba mizigo."
Mama Rehema alimtazama mwanawe kwa macho yenye upendo na wasiwasi. Tangu baba yao alipofariki miaka mitatu iliyopita, Juma alikuwa amejichukulia jukumu la kuisaidia familia. Lakini mama alijua moyoni mwake kwamba mtoto huyu alikuwa na ndoto kubwa zaidi ya kubeba mizigo sokoni.